Mkoani FM

Wanahabari Pemba watakiwa kuibua changamoto za wananchi

5 October 2023, 10:23 am

Mratibu wa mradi wa Kataa Udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Kusini Pemba Zulekha Maulid Kheri (Picha Khadija Rashid)

Waandishi wahabari kisiwani Pemba wametakiwa kusaidia jamii kupambanana  na udhalilisha wa aina yoyote ile  sambamba na kutoa elimu juu ya vitendo hivyo  ambavyo bado vimo ndani ya jamii.

Na Khadija Rashid         

Jumuiya ya KUKHAWA  kisiwani Pemba imezitaka kamati za kuibua changamoto za kijamii wakiwemo waandishi  wa habari kuendeleza kazi zao ili kuibua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuzitangaza katika vyombo vyao vya habari.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa mradi wa Kataa Udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Kusini Pemba Zulekha Maulid Kheri ofisini kwao Chake Chake kisiwani humo wakati wa kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa kamati hizo.

Amewataka waandishi wa habari kutokodolea macho kuripoti kesi za udhalilishaji wa kingono pekee bali waielimishe jamii iliyowazunguka kuwa udhalilishaji uko wa aina mbalimbali ikiwemo ajira za watoto, hivyo wananchi wana wajibu wa kutoa ushirikiano na taasisi husika kuziripoti pale  zinapotokea kwani zinawakosesha haki za msingi wale wanaofanyishwa kazi ikiwemo elimu.

Mratibu huyo  amewataka wazazi kuondoa woga na mapenzi makubwa kwa watoto wao badala yake wawafunze katika makuzi ya maadili mema na kujilinda na vitendo viovu na hilo lote linaweza kufanyika iwapo wazazi watachukua wajibu wao.

Hata hivyo wadau wa jumuiya hiyo  wamewashauriwa  waandishi  wa habari kujenga utamaduni wa  kwenda kutafuta na kuandika habari zinazowakwaza wananchi walioko  vijijini badala ya kusubiri habari za kulishizwa na watu.

Wamesema vijijini kuna taarifa nyingi ambazo zinapaswa kuandikwa kwenye vyombo vya habari hususani za wimbi la udhalilishaji wa kijinsia ambalo limekuwa likiendelea kwa kukabiliwa na changamoto mbali mbali lakini wanashindwa kuzipeleka kunako husika kwa madai hawaelewi waandishi watawapata wapi.

Wadau hao wamesema wana hamu na waandishi wa habari watembelee katika maeneo yao mbalimbali ya vijijini kwani kuna mambo mengi ambayo wanahitaji kupelekewa mbele na kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwa vile sauti za wanahabari zinafika mbali sana.

Wadau hao walieleza kuwa wanayo mambo mengi ambayo wanahitaji kuyaeleza kwa waandishi wa habari ikiwemo kukosekana kwa uwajibikaji  kwa baadhi ya watendaji wa serikali hivyo waandishi watakapofika katika maeneo yao kiu yao itaondoka  kwa vile sauti zao zitasikika.

Mshiriki  Maulid Kheri Ramadhan aliwataka waandishi wa habari kutokuwa waoga kufika vijijini kwani wananchi wana hamu ya kuwaona, kwani wana dukuduku nyingi ambazo hawana pa kuzieleza ikiwa sio kwa vyombo vya habari hususani kesi za udhalilishaji na hukumu zinavyotoka.

Hata hivyo Mkurugenzi wa jumuiya  ya KUKHAWA  , Hafidh Ali Said alizitaka kamati za ufuatiliaji kuendelea kufanya  kazi zao ili kuweza kuibua changamoto za kijamii katika shehia husika kwani nia ya jumuiya ni kuona kumekuwa na mafanikio.