Mkoani FM

Rushwa ya ngono chanzo ushiriki mdogo wa wanawake katika uongozi, maamuzi

3 June 2025, 10:18 pm

Kuwepo kwa vitendo vya rushwa ya ngono vinavyowakumba baadhi ya wanawake wakati uchanguzi ni moja ya sababu zinazopelekea kundi hilo  kutofikia lengo la kuwa kiongozi na kufanya kuwa na ushiriki mdogo katika uongozi na ngazi za maamuzi.

Wakizungumza na mwandishi wa Habari hizi baadhi ya wananchi shehia ya Jombwe Wilaya Mkoani wamesema wapo wanawake wenye nia ya kuwa viongozi lakini kinachokwamisha ni baadhi ya watu kutumia fimbo ya Rushwa ya ngono kuwarejesha nyuma na harakati hizo.

Akitoa ushuhuda mmoja wa mwanamke (jina linahifadhiwa) aliekutana na changamoto ya rushwa ya ngono wakati wa kuingia katika harakati za uongozi amesema changomoto hiyo ilimfanya akate tamaa na kushindwa kuendeleza ndoto yake ya kuwa kiongozi.

Kwa upande wake kaimu mratibu wa chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar Amina Ahmed Moh’d amesema tamwa inaendelea kutoa elimu kwa wanawake ili kuvitambua viashiria vya udhalilishaji pamoja na kuripoti sehemu husika ili haki inatendeke na waweze kufikia lengo la kuingia katika uongozi.

Afisa Elimu kwa umma kutoka Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar Sada Salum amesema bado jamii haijawa na muamko wa kuripoti kesi hizo sehemu husika kutokana na kuona aibu jambo ambalo linawakosesha haki zao za kimsingi.

Ameeleza kuwa miongoni mwa hatua wanazozichukua nikuelimisha jamii kupitia vyombo vya Habari na mikutano katika shehia, kuonesha athari ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa chaguzi na hatua za kuchukua mtu ambae atafikwa na kazia hiyo.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifung cha 21. (1) kimeeleza Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia Wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari.

Sheria ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar sheria namba 5 ya mwaka 2023 kifung cha 50 (1) kimeeleza mtu ambae anatoa rushwa kwa mtu mwengine ikiwa ya moja kwa moja au vyenginevyo kwa lengo la kumshawishi mtu huyo au mtu mwengine yoyote kupiga kura au kuacha kupiga kura ametenda kosa kisheria.