Wanahabari Pemba waaswa kusoma sheria zao
16 December 2024, 2:16 pm
Licha ya uwepo wa uhuru wa habari duniani lakini bado sheria za habari zinazotumika Zanzibar zinaonekana kubana wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.
Na Khadija Ali.
Waandishi wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kuzisoma na kuzifahamu Sheria za habari lengo kujua mapungufu yaliyomo.
Zaina Abdulla Mzee Afisa Mradi wa sheria za Habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)_Zanzibar amesema ni muhimu kwa waandishi kuzisoma na kuendelea kuzifanyia uchechemuzi Iengo kupatiwa ufumbuzi.
Akiwasilisha mada juu ya uhuru wa habari Mkurugenzi Mshauri kutoka TAMWA_Zanzibar Haura Shamte amesema ni muda wa miongo miwili sasa wanaharakati wanapigania uwepo wa sheria rafiki za habari lakini bado hazijapatiwa ufumbuzi.
Ameongeza ni wajibu kwa wanahabari kuendelea kupaza sauti zao ili sheria mpya za habari zipatikane na kuleta mabadiliko katika tasnia hiyo na nchi kwa ujumla.
Nao wandishi walioshiriki mafunzo hayo wamesema umefika wakati kuwepo kwa sheria mpya za habari Zanzibar ili kuimarisha maendeleo ya tasnia ya habari.
TAMWA-Zanzibar wanaendelea kuvijengea uwezo vyombo vya habari ili kuandika makala na kutengeneza vipindi vya uchechemuzi kwa lengo la kupatikana kwa sheria mpya za habari Zanzibar.
Sheria zinazodaiwa kuminya uhuru wa habari Zanzibar ni pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namb. 1 ya mwaka 2010, Sheria namb 5 ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 pamoja na marekebisho yake na Sheria namb 8 ya mwaka 1997.