Wenye ulemavu Pemba waomba kupatiwa fursa za kimichezo
21 May 2024, 4:08 pm
Jamii nchini imetakiwa kutoa ushrikiano katika kuwaunga mkono wanawake wenye ulemavu kwenye sekta ya michezo ili kuibua fursa zilizopo katika michezo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanawake hao wanaojishughulisha na harakati za michezo wilaya ya Mkoani Bi. Fatma Mohd kutoka shehia ya Kangani na Mariam Hamad Ali kutoka shehia ya Uweleni wachezaji wa mpira wa wavu wamesema bado jamii haijawa tayari kutoa ushirikiano katika kundi la watu hao jambo ambalo linawakosesha fursa hiyo muhimu.
Wamesema watu wenye ulemavu wana fursa sawa ya kushiriki katika michezo kama kundi lingine hivyo ni vyema kutoa fursa na mashirikiano katika kundi hilo ili kuonesha vipaji vilivyopo kwa watu wa kundi hilo.
Afisa watu wenye ulemavu wilaya ya Mkoani Wardat Walii Mohd amesema licha ya kuwepo kwa fursa ya kundi hilo kushiriki katia michezo lakini wanakabiliwa na changoamoto ya rasilimali fedha pamoja na rasilimali za vifaa kwa watu wa kundi hilo jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kuliibua kundi hilo katika michezo.
Kwa upande wake Juma Said Mohd katibu wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Mkoani amesema licha ya kuwepo fursa sawa lakini hawajawa na timu maalum ya watu wenye ulemavu isipokuwa wanalazimika kuwachukua wanawake wenye ulemavu kutoka sehemu mbalimbali ndani ya wilaya ya Mkoani ili kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimichezo.