Mkoani FM

Katibu Machigini: wakulima ongezeni bidii kuondoa uhaba wa chakula

21 September 2022, 11:47 am

Baadhi ya Wakulima na Viongozi wao wa Bonde la Machigi Wilaya ya Mkoani Pemba

 

Wakulima  wa  kilimo cha umwagiliaji wa bonde la machigini, shehia ya mjimbini  Mkoani Pemba wameshauriwa   kuongeza bidii kwenye kilimo chao cha mpunga kwa lengo la kuongeza kasi ya uzalishaji .

Ushauri huo umetolewa na katibu wa bonde hilo,Hamdu Hassan Bakari wakati   wa mkutano na wakulima hao,  wenye lengo la kujadili jinsi gani wataweza kuongeza uzalishaji katika ukulima wao ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa chakula ambapo taaluma ya kilimo cha kisasa walionayo inaweza kusaidia kufikia malengo hayo.

Amesema wakati umefika kwa  wakulima kuacha kulima kwa mazoea na badala yake wafuate maelekezo ya wataalam (mabwana shamba)ili kuongeza kasi ya uzalishaji na  kujikwamua na hali duni za kiuchumi pamoja na kuongeza pato la taifa kwa jumla.

Hasina Ali Mussa na Issa Nassor Issa  miongoni mwa wakulima wa bonde hilo  wamesema  licha ya juhudi wanazichukuwa kwenye kilimo chao cha mpunga lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa maji inayosababishwa na miundo mbinu, kutokua sawa kwa baadhi ya maeneo ya bonde hilo hali inayo waweka katika wakati mgumu kwani kilimo chao ni cha umwagiliaji zaidi.

Eneo la mashamba ka Bonde la Machigini

Wakulima hao hivi karibuni walipatiwa msaada   wa waya wa umeme  na watu wanaoishi nje ya nchi wanaotoka Wilaya  ya Mkaoni kwa ajili  kurudisha  huduma ya maji ili wapate kuendelea  shughuli zao za umwagiiaji  baada ya kuibiwa waya wao wa mwanzo katika bonde hilo.

Aidha wameiomba  Wizara ya kilimo kupitia idara ya umwagiliaji kufika katika bonde lao mara kwa mara ili kuwatatulia changamoto zinazowakabili kama vile kuwapatia wataalamu wakilimo pamoja na vifaa vya kisasa ili kuongeza uzalishaji.

Bonde la machigini lina jumala ya wakulima 200 ambao wanajishughulisha na kilimo cha  mpunga wa umwagiliaji  na mazao mengine ya biashara kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.