Highlands FM
Highlands FM
10 March 2026, 14:56

Wataalamu wa afya wanatoa tahadhari kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia mswaki kwa muda mrefu kupita kiasi, wakieleza kuwa kubadilisha mswaki mara kwa mara ni muhimu katika kulinda afya ya meno na kinywa pamoja na kuzuia magonjwa yanayoweza kujitokeza.
Na Mwanaisha Makumbuli
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa bado wanatumia mswaki kwa muda mrefu zaidi ya mwezi mmoja kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya kiuchumi na ukosefu wa uelewa kuhusu muda sahihi wa kubadilisha mswaki.
Wananchi hao wamesema mara nyingi hubadilisha mswaki baada ya kuharibika kabisa, hali inayowafanya kutumia mswaki mmoja kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Meno na Kinywa, kutoka hospital ya Mbalizi ifisi SIAEL NNKO amesema ni muhimu kwa kila mtu kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku, kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya fluoride ili kusaidia kulinda meno dhidi ya kuoza na kubadilisha mswaki mara kwa mara ili kulinda afya ya meno na fizi.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya floridi ili kusaidia kulinda meno dhidi ya kuoza.
Daktari huyo pia alitoa wito kwa jamii kuendelea kutafuta elimu ya afya ya kinywa na meno pamoja na kufika hospitalini mara kwa mara kwa uchunguzi wa meno ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye.