Highlands FM

Bango la Amri Kumi za Mungu Mafyati lavuta hisia

9 July 2025, 11:42

Amri Kumi za Mungu.Picha Samwel Mpogole

Jamii imetakiwa kusoma na kuzielewa Amri Kumi za Mungu katika kufanya matendo mema.

Na Samwel Mpogole

Katika hali isiyo ya kawaida lakini yenye ujumbe mzito wa kiroho na maadili, kundi la watu limeweka bango lenye Amri Kumi za Mungu katika eneo la Mafyati Jijini Mbeya – eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitajwa kwa mienendo inayodaiwa kuwa ya kukiuka maadili, hasa nyakati za jioni.

Philimon Ngunge ni mmoja wa waumini waliobeba jukumu la kusimamisha bango hilo. Anasema hatua hiyo imelenga kuwakumbusha wakazi wa eneo hilo na wapita njia kuhusu thamani ya maadili mema na kumcha Mungu.

“Tuliona kuna haja ya kutoa ujumbe huu kama njia ya kutubu kwa niaba ya jamii yetu, lakini pia kuwaalika watu kutafakari namna wanavyoishi,”

Sauti Philimon Ngunge

Wakazi wa eneo hilo na baadhi ya wapita njia wamepokea bango hilo kwa mitazamo tofauti. Wapo waliolipongeza wakisema ni hatua nzuri ya kurudisha maadili, huku wengine wakisema kinachohitajika ni elimu na si mabango pekee.

“Ni vizuri sana. Angalau sasa watu wakipita wasome na wajitafakari. Siyo kila kitu burudani na starehe tu,” amesema mkazi mmoja 

“Kwangu naona ni wazo zuri, lakini zaidi ya bango, tunahitaji semina au mikutano ya kijamii ya kutuelimisha,” amesema mwingine.

Sauti ya Wananchi

Eneo la Mafyati limekuwa likitajwa mara kadhaa kwa tabia za baadhi ya wadada “kujikuza” au kujionyesha kwa namna isiyo ya kawaida hasa nyakati za jioni jambo ambalo limeibua mjadala mkubwa kuhusu maadili miongoni mwa jamii.

Kwa sasa, bango hilo linaendelea kusimama kama ukumbusho wa kiroho na sauti ya wito wa mabadiliko kwa jamii ya Mafyati na Mbeya kwa ujumla.