Highlands FM
Highlands FM
1 July 2025, 12:41

Utalii unachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa la Tanzania kwa mwaka 2016 ambapo sekta hii inakua kwa kasi, ikipanda kutoka dola bilioni 1.74 mwaka 2004 hadi dola bilioni 4.48 mwaka 2013.
Na Samwel Mpogole
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase, amesema maandalizi ya Tamasha la Mpalano Festival linalotarajiwa kufanyika tarehe 6 hadi 7 Julai 2025 yamekamilika, akieleza kuwa dhamira kuu ya tamasha hilo ni kuinua sekta ya utalii, kuenzi mila na desturi, pamoja na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Kyela na mikoa jirani.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Highlands FM radio, DC Manase amesema Mpalano Festival ni jukwaa mahsusi la kuonesha urithi wa kiutamaduni wa Kyela, hususan ngoma za asili, vyakula vya kiasili, mavazi ya kitamaduni, na historia ya watu wa Kyela, huku likifungua milango kwa wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Aidha, DC Manase ametoa wito kwa wananchi wa Kyela na wageni kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo, akisisitiza kuwa mbali na burudani, Mpalano Festival ni jukwaa la kuunganisha jamii, kukuza uchumi na kutangaza vivutio vya pekee vilivyopo wilayani humo kama vile ziwa Nyasa, mito yenye maji ya moto na mandhari ya kipekee ya kijani kibichi.
Mpalano Festival mwaka huu linatarajiwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi, huku likipambwa na maonesho ya bidhaa, mashindano ya ngoma, na midahalo ya vijana kuhusu maendeleo ya jamii sambamba na kutembelea vivutio.