Highlands FM

Mafunzo ya urekebishaji gerezani  yatoa tumaini kwa wafungwa

19 June 2025, 08:07

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa. Picha na Samwel Mpogole

Wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi wakiwa gerezani  wahimzwa tabia njema wakimaliza vifungo

Na Samwel Mpogole

Jeshi la Magereza nchini limeendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa wafungwa, ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea mara baada ya kumaliza vifungo vyao.

Akizungumza katika mahafali ya wahitimu, Naibu Kamishna wa Magereza, Ahmad Mwen-Dadi, ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Urekebu, amesema kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya ujuzi kama njia ya kuwainua wahitimu kiuchumi na kijamii.

Sauti ya Ahmad Mwen-Dadi

Nao baadhi ya walimu wa wafungwa hao wamesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa wahusika, wakiashiria mienendo na dhamira mpya iliyojitokeza kwa wahitimu baada ya kupewa ujuzi.

Sauti ya walimu wa wafungwa

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, aliyewakilisha Mkuu wa Mkoa, Dkt. Juma Homera, amewataka wahitimu kutumia maarifa waliyopewa kama njia ya kuachana na uhalifu na kujipatia kipato halali baada ya kifungo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Beno Malisa

Katika mafunzo haya, jumla ya wafungwa 81 walianza, lakini 73 pekee ndio waliohitimu, baada ya wengine 8 kushindwa kuendelea kutokana na changamoto mbalimbali. Mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na. Ufundi umeme, Useremala, Upakaji rangi, Ufundi bomba, Uwashi,Uchomeleaji na Ubunifu wa mitindo.

Wahitimu wameiomba serikali na wadau kuendelea kuwapatia vitendea kazi watakapotoka gerezani ili waweze kutumia stadi hizo kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii zao. Mahafali haya yamebebwa na kaulimbiu isemayo:“Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya ni Msingi wa Mafanikio ya Urekebu.

Naibu Kamishna wa Magereza, Ahmad Mwen-Dadi. Picha na Samwel Mpogole