Highlands FM
Highlands FM
12 June 2025, 17:28

Matumizi ya mkaa na kuni yatajwa kuhatarisha maisha ya wakazi wa Mbeya na Njombe wakati wa baridi kali
Na Samwel Mpogole
Wakati mikoa ya Mbeya na Njombe ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa hali ya hewa ya baridi kali nchini, wakazi wa mikoa hiyo wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kujipatia joto katika msimu huu wa baridi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Dkt. Joyce Massaro, bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, akizungumza na Highlands FM ofisini kwake amesema matumizi ya mkaa na kuni katika mazingira ya ndani yanaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu, hasa watoto na wazee.
“Matumizi ya nishati hizi hutoa moshi wenye kemikali hatari ambazo husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji, kama vile kikohozi cha muda mrefu, pumu na hata magonjwa sugu ya mapafu,” amesema Dkt. Massaro .
Katika hatua nyingine, Dkt. Massaro ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata joto kwa njia salama zaidi badala ya kutumia kuni na mkaa.
“Ni muhimu kutumia mavazi yenye joto kama sweta, soksi na mablanketi mazito kuwakinga watoto na baridi. Pia usafi wa mazingira unapaswa kuzingatiwa ili kuzuia magonjwa ya mlipuko na ajali ndogondogo zinazoweza kusababishwa na moto wa kuni au mkaa,” ameongeza.
Nao baadhi ya wananchi wa Jiji la Mbeya wameeleza namna wanavyokabiliana na baridi kali, huku wakieleza changamoto wanazokutana nazo katika kuhakikisha familia zao zinabaki salama.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa mikoa ya Mbeya na Njombe inakabiliwa na baridi kali kwa sasa, ambapo mkoa wa Mbeya umerekodi wastani wa nyuzi joto za juu 23°C na za chini 9°C. Hali ni kali zaidi mkoani Njombe ambako kiwango cha juu ni nyuzi 17°C na cha chini ni nyuzi 9°C.
Kwa mujibu wa TMA, hali hii ya baridi inatarajiwa kuendelea kwa wiki kadhaa, hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki za kujilinda kiafya.