Highlands FM
Highlands FM
11 June 2025, 16:33

Waandishi wa habari Mbeya waaswa kujiandaa kwa maisha baada ya utumishi
Na Samwel Mpogole
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani Mbeya wamepewa mafunzo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii pamoja na kuwa mabalozi wa kuelimisha umma juu ya maandalizi ya maisha ya kustaafu.
Mafunzo hayo yamefanyika jijini Mbeya katika ukumbi wa Mgwasi, yakihusisha majadiliano ya kina kati ya wataalamu wa PSSSF na wanahabari kuhusu umuhimu wa kuwa na maandalizi bora ya baada ya utumishi ambapo Meneja wa PSSSF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ramadhani Mgaya na Afisa Mahusiano kutoka Makao Makuu ya PSSSF Dodoma, Rehema Mkamba Wameeleza nafasi ya waandishi wa habari katika kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa umma
Kwa upande wake, mmoja wa wanachama wa PSSSF ambaye pia ni mstaafu, Vicent Msola, ameshuhudia kwa namna mafao yake yalivyopatikana kwa haraka baada ya kustaafu, jambo linaloonesha ufanisi wa mfumo huo.
Naye Mweka Hazina wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mbeya (Mbeya Press Club), Bi. Rukia Chasanika, amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa wanahabari, hasa kwa kuwaongezea uelewa juu ya haki na wajibu wao katika hifadhi ya jamii.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wadau mbalimbali, wakiwemo wanahabari ambao wana mchango mkubwa katika kuibadilisha jamii kupitia taarifa.