Highlands FM

Polisi Mbeya latoa onyo kwa madereva wazembe

10 June 2025, 18:14

ASP Hezron Mkangi. Picha na Samwel Mpogole

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limetoa onyo kali kwa madereva wazembe kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuzuia ajali na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara

Na Samwel Mpogole

Siku moja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linasimamia ipasavyo sheria za usalama barabarani ili kudhibiti ajali, jeshi hilo mkoani Mbeya limetangaza msimamo wake dhidi ya madereva watakaokiuka sheria hizo.

Agizo hilo la Rais limetolewa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika eneo la Mlima Iwambi, Wilaya ya Mbeya, ambapo watu 28 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Akizungumza kupitia kipindi cha Darubini kilichorushwa na kituo hiki, Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Mbeya, ASP Hezron Mkangi, amesema jeshi hilo litaendelea kusimamia sheria kwa weledi ili kulinda usalama wa watumiaji wa vyombo vya moto pamoja na watembea kwa miguu.

Sauti ya ASP Hezron Mkangi

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi Michael Mduda kutoka Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani, ofisi ya mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa  Mbeya amesema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakikaidi sheria, hasa kwenye maeneo ya vivuko vya waenda kwa miguu pamoja na yale yenye taa za kuongozea magari, jambo linalochangia ajali.

Sauti ya INSP Michael Mduda

Naye Sajini Taji, Felisier Mheza, kutoka dawati hilo hilo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanaposhuhudia ukiukwaji wa sheria, ili kusaidia juhudi za kudhibiti ajali na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.

Sauti ya S/SGT Felisier Mheza

Jeshi la Polisi limehimiza kuwa mafanikio ya kudhibiti ajali barabarani yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka na wananchi katika kufuata sheria na kutoa taarifa kwa wakati.