Highlands FM
Highlands FM
3 June 2025, 19:14

Wananchi wa Mbeya walia na ukosefu wa vivuko salama wakati ujenzi wa barabara ya njia nne ukiendelea
Na Samwel Mpogole
Wakati ujenzi Barabara ya njia nne ukiendelea jijini Mbeya, Baadhi ya wananchi wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya njia mbadala ikiwemo vivuko, ili kuwarahisishia watembea kwa miguu kuendelea na shughuli bila kukumbana na vikwazo vya msongamano wa magari.
Wananchi hao wanasema kuwa pamoja na umuhimu wa mradi huo wa kimkakati, zipo changamoto mbali mbali katika miundombinu ya kupita kwa miguu, vivuko, na njia mbadala kuelekea katika makazi na ofisi zao.
Mradi wa barabara hiyo una urefu wa kilomita 29 na unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 138.7, chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania – TANROADS. Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Matari Masige , ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mradi huo, ametoa ufafanuzi kuhusu changamoto zinazolalamikiwa na wananchi.
Mhandisi Maige pia amethibitisha kuwa kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo, tayari hatua imechukuliwa na muda wa utekelezaji umeongezwa kwa miezi sita ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa viwango na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Barabara ya njia nne ya Mbeya inatarajiwa kuboresha mtandao wa usafiri na kukuza uchumi wa mkoa huo kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, ushirikishwaji wa wananchi na uboreshaji wa miundombinu ya vivuko na njia salama, vinaendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayosisitizwa ili mradi huu uwe wa manufaa kwa wote.