Highlands FM
Highlands FM
2 June 2025, 14:30

Wazazi na walezi watakiwa kuwa makini na watoto wao katika matumizi ya mitandao ya kijamii ili kulinda maadili na afya ya akili za watoto hao dhidi ya athari zinazoweza kutokana na matumizi mabaya ya teknolojia.
Na Samwel Mpogole
Katika kipindi hiki ambacho matumizi ya mitandao ya kijamii yameongezeka kwa kasi, wazazi na walezi wametakiwa kuwa makini na kuwasimamia watoto wao, ili kuwalinda dhidi ya athari za kimaadili na kisaikolojia zitokanazo na matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.
Wito huo umetolewa na Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Bi. Betuna Mwamboneke, alipokuwa akizungumza na Highlands FM kuhusu hali ya ongezeko la maudhui hatarishi kwa watoto kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wao, viongozi wa dini Mchungaji Christopha Mkama wa Kanisa la Waadventista Wasabato na Shehe Hasan Katanga Mjumbe wa Baraza la Mashekhe Mkoa wa Mbeya
wamesema wana nafasi ya kipekee kusaidia jamii kuelewa madhara ya matumizi mabaya ya mitandao, hasa kwa watoto na vijana.
Nao baadhi ya wananchi wametoa maoni yao wakisema wameanza kubadilika katika namna wanavyosimamia watoto wao, huku wakitaka elimu hiyo itolewe zaidi mashuleni na katika nyumba za ibada.
Taarifa zinaeleza kuwa ongezeko la matatizo ya afya ya akili kwa watoto linaweza kuhusishwa moja kwa moja na matumizi yasiyodhibitiwa ya mitandao, ikiwemo upatikanaji wa taarifa zisizofaa kwa umri wao.