Highlands FM
Highlands FM
26 May 2025, 15:33

Baadaya ya mbunge wa Mbeya mjini kutangaza nia kuelekea kugombea uyole makada wa CCM wameanza kutangaza nia kuchukua kijiti chake.
Na Samwel Mpogole
Siku chache baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, kutangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Uyole, makada wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kupigana vikumbo kuwania tiketi ya ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini.
Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba, pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mbeya, Charles Mwakipesile, ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho.
Akizungumza kuhusu nia yake ya kuwania ubunge, Nsomba amesema amejipima na kuona ana uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Mbeya Mjini, hasa baada ya Dk. Tulia kuelekeza nguvu zake Jimbo la Uyole.

Charles Mwakipesile. Picha na Mwandishi wetu.
Kwa upande wake, Mwakipesile amesema anakusudia kuchukua fomu rasmi tarehe 28 Juni, sambamba na makada wengine watakaowania nafasi hiyo kupitia CCM.
Mvutano huu wa kisiasa unakuja baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza kugawanywa kwa Jimbo la Mbeya Mjini, na kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Uyole. Tarehe 23 Mei, Dk. Tulia alitangaza rasmi nia ya kuwania jimbo hilo jipya.