Highlands FM

Wawili wahukumiwa miaka 30 jela kwa ubakaji Mbeya

19 May 2025, 19:15

Mwandishi Samweli Mpogole

Mahakama ya Wilaya ya Chunya imemhukumu Lutenga Wilson Majora (32), mkazi wa Kitongoji cha Itumbi, Kata ya Matundasi, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 ambaye alikuwa akiishi naye kinyumba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamini Kuzaga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamini Kuzaga akizungumza na waandishi wa habari, amesema. Tukio hilo lilifichuliwa na raia mwema na kufikishwa kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Chunya mnamo Mei 14, 2024.

Baada ya kupokea taarifa hizo, uchunguzi ulifanyika haraka na tarehe 15 Mei 2024 mtuhumiwa alikamatwa akiwa na mtoto huyo na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Chunya.

“Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi kama mke wa mtuhumiwa kwa muda. Uamuzi wa mahakama umetolewa baada ya ushahidi wa kutosha kuwasilishwa,” alisema RPC Kuzaga.

Katika tukio jingine, Mahakama ya Wilaya ya Mbarali imemhukumu Kurwa Memba (30), mkazi wa Kijiji cha Lukali, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), mkazi wa Kigoe-Kapyo, kata ya Mahongole.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, msichana huyo alitoroshwa na mtuhumiwa na kupelekwa jijini Dar es Salaam ambapo alitambulishwa kama mke wake. Tukio hilo liliibua masikitiko makubwa kutokana na mazingira ya unyanyasaji na udhaifu wa msichana huyo.”Kitendo hiki si tu ni kosa la jinai bali pia ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya watu wenye ulemavu.

Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaowatendea watoto vitendo vya ukatili,” alisisitiza RPC wa Mkoa wa Mbeya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuhimiza ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake ili kuhakikisha jamii inakuwa salama kwa wote.