Tumbatu FM
Tumbatu FM
29 November 2026, 07:12

” Hakikisheni vijana wakimbiza mwenge wa uhuru mwaka 2027 wanakuwa na sifa zinazostahili na kwenye uwezo wa kufanya hazi hiyo kwa weledi”
Na Salama Mbarouk Khatibu
WAZIRI wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji, Ali Suleiman Ameir “Mrembo”, amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Wizara husika kuhakikisha vijana watakaoteuliwa kushiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2027 wanakuwa na sifa zinazostahili, pamoja na kupatiwa mafunzo ya kutosha kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa tathmini ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 uliofanyika katika ukumbi wa Madinat Al Bahari, Bweni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, Waziri Mrembo amesema maandalizi ya mapema na uchaguzi makini wa vijana ni muhimu katika kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi na kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Ameema mkutano huo ni fursa muhimu kwa washiriki waliokuwa sehemu ya usimamizi na ukimbizaji wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 kujadili mafanikio, mapungufu na changamoto zilizojitokeza, ili kuweka mikakati madhubuti ya kuimarIsha maandalizi na utekelezaji wa mbio hizo kwa mwaka 2027.
Waziri Mrembo amewashukuru viongozi, watendaji na vijana wote walioshiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, kuanzia mwanzo wa safari hiyo hadi kilele chake, akisema ushirikiano wao umechangia kufanikisha zoezi hilo.
Aidha, amewataka wakuu wa Mikoa na Wizara zinazohusika kuhakikisha wanakuwa na maandalizi ya kutosha katika mchakato wa kuomba na kuchagua wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2027.
Amesisitiza umuhimu wa kuwazingatia vijana wenye sifa, uwezo, nidhamu na utayari wa kutekeleza majukumu hayo.
Amesema kuwapatia mafunzo vijana kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho wa uteuzi kutasaidia kuwajengea uelewa wa majukumu yao, historia na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru, pamoja na matarajio ya zoezi hilo kwa Taifa.
Mkutano huo wa tathmini umekusudia kupitia kwa kina namna mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zilivyosimamiwa, kubaini changamoto zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuweka mikakati itakayosaidia maandalizi ya mbio za mwaka 2027 kuwa bora zaidi.
Wakitoa shukrani zao katika mkutano huo, viongozi wa mikoa na wilaya za Kaskazini Unguja na Pemba walieleza kuridhishwa na ushirikiano uliotolewa na wadau mbalimbali wakati wa mbio hizo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo katika maandalizi yajayo.
Wamesema tathmini hiyo itasaidia kuimarisha uratibu wa shughuli za Mwenge wa Uhuru, kuimarisha mawasiliano baina ya viongozi na watendaji, pamoja na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.