Tumbatu FM
Tumbatu FM
3 March 2026, 10:43

“Kunahaja ya kuleta walimu wa usalama wetu kwanza kwaajili ya kutoa elimu kuhusu udhalilishaji kwa shule za Tumbatu ili kuwanusuru watoto na janga hili matukio mengi yamekua yakitokeza ingawa hayaripotiwi”
Na Vuai Juma.
Dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja limepanga kupeleka walimu wa usalama wetu kwanza katika skuli za Tumbatu ili kutoa elimu kuhusu masuala ya udhalilishaji wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa dawati hilo Inspector wa polisi Salum Khamis Machano wakati wa kikao cha Pamoja kati ya walimu wa skuli ya sekondari Tumbatu Pamoja na kamati ya wazazi kuhusu changamoto ya ukatili wa kijinsia kisiwani humo.
Amesema wamepokea malalmiko kutoka kwa wasamaria wema kuhusu kuwepo kwa baadhi ya watu wa eneo hilo wanaofanya vitendo vya kuwadhalilisha watoto jambo ambalo limewafanya kuweka mikakati itakayopelekea kuliondosha tatizo hilo ikiwemo kuwapeleka polisi watakaosaidiana na walimu kutoa taaluma kwa wanafunzi.
Aidha amewataka wazazi kuwa na tabia ya kufuatilia mienendo ya watoto wao Pamoja na kutowapa uhuru wa kupitiliza jambo ambalo hupelekea kuongezeka kwa matendo mabaya.

Kwa upande mwengine mwenyekeiti wa kamati ya wazazi skuli ya sekondari Tumbatu Mwalim Ngwali Makame Kire amaekiri kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji katika
jamii huku akisema changamoto kubwa ni kutoviripoti kwa mamlaka husika kutokana na ukaribu wa kifamilia.
Nao wajumbe wa kamati hiyo wameliomba jeshi la polisi kuharakisha upatikanaji wa walimu wa usalama wetu kwanza sambamba na kuipeleka elimu kwa walimu wa madrasa.