Tumbatu FM
Tumbatu FM
25 November 2026, 14:34

“Sina shaka ifikapo 2030 ajira 350,000 zinakwenda kuzaliswa.”
Na Sauda Silima Khamis
WAZIRI wa Kazi, Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Ali Suleiman Ameir, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha vijana na wanawake kujiajiri, kukuza ubunifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili kujenga uchumi imara na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Amesema hayo katika Hotel ya Zanzibar Beach Resort wakati akizindua Mradi Jumuishi wa Uwezeshaji Kiuchumi kwa Vijana na Wanawake Zanzibar (Economic Inclusion Youth and Women in Zanzibar), unaotekelezwa na taasisi ya Zanzibar Fighting Against Youth Challenge Organization (ZAFAYCO), wenye thamani ya dola za Marekani milioni 2.72, unaolenga kuwafikia vijana 3,000 kutoka Unguja na Pemba.
Amesema mpango huo umefika wakati mwafaka kutokana na umuhimu wa kuwapatia vijana na wanawake ujuzi, maarifa na mitaji itakayowawezesha kujitegemea kupitia ajira na shughuli za ujasiriamali.
Amesema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya uwezeshaji, ikiwemo kupitia Sera ya Vijana ya mwaka 2005 na kuanzisha sera mpya ya mwaka 2023 inayoweka mkazo katika elimu, ujuzi, ubunifu na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya taifa.
Ameongeza kuwa serikali imejiwekea kuzalisha ajira 350,000 ifikapo mwaka 2030 akieleza kuwa fursa hizi zitazingatia utu, heshima na silka za wazanziar.
Ameir amesema fursa hizo za ajira zitatokana na njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na mfuko wa fedha wa Inuka, Hakika na Dr. Mwinyi Business Fund pamoja na mifuko mingine inayosimamiwa na wadau na wapenda maendeleo waliopo Nchini
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdalla amewataka vijana na wanawake kutumia fursa zinazotolewa na mradi huo kujenga ujuzi, kupata mitaji na kuanzisha shughuli zitakazoboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Amesema Mkoa wa Mjini Magharibi una umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa programu hiyo kutokana na idadi kubwa ya vijana na wanawake.
Amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinazoonesha kuwa mkoa huo una wakazi 893,169, sawa na asilimia 47.3 ya wakazi wote wa Zanzibar.
Amesema wanawake wanachangia asilimia 52.1 ya wakazi wa mkoa huo, huku vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wakiwa asilimia 39.1, ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 34.4.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ZAFAYCO, Rukia Hamdani Abdalla, amesema mafanikio ya mradi yanapaswa kupimwa kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya wanufaika badala ya kuangalia idadi ya shughuli zilizofanyika au fedha zilizotumika.