Tumbatu FM

SUZA yazindua maadhimisho ya miaka 25 ya elimu

6 October 2026, 21:27

Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Said Ali Hamad Vuai wakati akizungumza na waandishi wa habari, Picha Mwandishi waetu (kutoka Suza)

“Tutajitahidi kuwa na matukio rafuki yenye nafasi ya kuhusisha makundi mbali mbali ya jamii ili sherehe hizi ziwe za aina yake na zenye kuvutia”

Na Juma Haji

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimezindua rasmi maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo, yanayolenga kusherehekea safari ya mafanikio, yaliyopatikana pamoja na hatua mbalimbali za maendeleo zilizofikiwa katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya SUZA, Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema maadhimisho hayo yatahusisha matukio mbalimbali ya kitaaluma, kijamii, michezo na maendeleo yatakayowashirikisha wanajumuiya wa SUZA pamoja na jamii kwa ujumla.

Ametaja baadhi ya matukio yatakayofanyika katika kipindi cha maadhimisho hayo amesema SUZAitasoma dua maalumu ya kuwaenzi wanajumuiya wa SUZA waliotangulia mbele ya haki, matembezi ya hisani, bonanza la michezo, makongamano, Wiki ya Kiswahili, shughuli za kijamii maonesho ya utafiti na ubunifu, uzinduzi wa witendea kazi pamoja na mahafali ya chuo.

Sauti ya Prof. Said Ali Hamad Vuai ambae ni Makamu Mkuu wa Chuo, wakati akizungumza na waandishi wa habari

Amesema maadhimisho hayo yatahusisha pia shughuli za upandaji miti, usafi wa mazingira, huduma za afya ya kinywa na meno pamoja na kampeni mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kijamii.

Ametoa wito kwa jamii, wafanyabiashara, watu mashuhuri, Watanzania wanaoishi na nje ya nchi (Diaspora), wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na SUZA kwa kuchangia fedha katika ujenzi wa jengo la Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba.

Amesema ujenzi wa jengo hilo ni muhimu katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza uwezo wa Chuo kutoa programu za afya na sayansi za tiba na kuwawezesha wanafunzi kupata elimu hiyo Zanzibar, hatua ambayo itasaidia kupunguza gharama zinazoweza kuepukika za kusoma nje ya Zanzibar.

Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yamezinduliwa rasmi leo, tarehe 6 Oktoba 2026, na yatahusisha shughuli mbalimbali zinazolenga kutafakari safari ya Chuo, kuonesha mafanikio yaliyopatikana na kuweka msingi wa hatua mpya za maendeleo kwa miaka ijayo.