Mkoani FM

RC Mattar aiomba Jukuruza kutoa elimu dhidi ya rushwa

7 August 2023, 11:14 am

Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud alipokutana na baadhi ya viongozi wa JUKURUZA ofisini kwake Chakechake Pemba. (Picha na Amina Masoud).

Baada ya wajumbe wa Jumuiya ya Kupinga Rushwa na Uhujumu Uchumi JUKURUZA kufika ofisi Mkoa Kusini Pemba kujitambulisha, Mkuu wa Mkoa huo Mattar Zahor Masoud ameiomba jumuiya hiyo kutoa elimu kwa wananchi ili kuondoa rushwa nchini.

Na Amina Masoud.

Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud ameitaka Jumuiya ya Kupinga Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar JUKURUZA,  kuendelea kutoa elimu ya rushwa kwa jamii kwani  kutapelekea kuokowa fedha nyingi na kuufanya uchumi  wa nchi uweze kukua.

Ameyasema hayo ofisini kwake wakati alipokuwa akizungumza na wanajumuiya hiyo mara baada ya kufika kwa ajili ya kujitambulisha na kusema kuwa kazi hiyo wanayoifanya watasaidia sana Serikali katika jitihada za mapambano ya kuondowa rushwa na uhujumu wa uchumi nchini.

Amesema bado jamii iko nyuma katika uelewa juu ya rushwa kwani hata mifumo ikiwemo ya kutolipa kodi ,kutodai risiti baada ya manunuzi  inapelekea mianya ya rushwa jambo ambalo linahitaji elimu kubwa kwa wananchi.

Mapema akitowa maelezo ya jumuiya hiyo Mratibu wa Jukuruza Pemba Juma Faki Mtumweni amesema lengo la jumuiya hiyo ni kutowa elimu kwa jamii ili waweze kujuwa athari na madhara ya rushwa.

Amesema kuwa imefikia wakati sasa baadhi ya watu huwadhalilisha wengine kwa sababu ya kupata maslahi yao binafsi jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya watu na serikali kwa ujumla.

Nae Mjumbe kutoka Wilaya ya Chakechake Ibrahim Mohamed Saleh amesema ni kweli kazi ya serikali ni nyingi na hivyo inahitaji juhudi kubwa kupitia wasaidizi mbalimbali  ikiwemo asasi za kiraia.

Akitowa shukrani kwa niaba ya jumuiya hiyo mjumbe kutoka wilaya ya Mkoani Salma Suleiman Abubakar aliahidi kushirikiana pamoja kati ya jumuiya hiyo na serikali kuhakikisha mafanikio ya kupinga rushwa yanafanikiwa.

Mwisho.