Wazazi wanatakiwa kuwaandikisha skuli watoto wao wenye ulemavu Pemba
26 October 2023, 9:36 am
Bado baadhi ya familia kisiwani Pemba wanawakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu watoto wao wenye ulemavu.
Na Khadija Ali
Wazazi na walezi kisiwani Pemba wametakiwa kuwaandikisha watoto wenye ulemavu skuli ili kupata haki yao ya msingi ya elimu kama watoto wengine.
Akifungua kongamano la Wadau wa Maendeleo Jumuishi katika Jamii CBID kilichofanyika katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake chake Pemba Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali amesema ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata fursa sawa ya elimu kama watu wengine wasio na ulemavu.
Ameeleza ulemavu wao isiwe sababu ya kuwakosesha haki zao kwani Serikali ya awamu ya nane imejitahidi kuimarisha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na kujenga skuli ambazo zimezingatia miundombinu rafiki kwa kundi hilo.
Akizungumzia lengo la Kongamano hilo Afisa utetezi wa Haki za Binaadamu kutoka taasisi ya Madrasa Early Childhood Nassir Rashid Ali amesema ni kuendelea kuwashajihisha wazazi kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wenye ulemavu katika jamii.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais, Ahmed Abuubakar Mohammed amezitaka Asasi za kiraia kujumuisha kundi la watu wenye ulemavu katika miradi yao ili wapate haki zao stahiki kama makundi mengine
Abdalla Shomari mwalimu wa elimu mjumuisho amesema badhi ya wazazi wanadhani kumuandikisha skuli mtoto mwenyeulemavu ni kumdhalilisha jambo ambalo si sahihi, na kuwataka wazazi kuacha dhana hiyo na badala yake wawajumuishe ili kupata msingi bora wa elimu wa hapo baadae.
Nao washiriki wa kongamano hilo Kasiim Ali Omar na Halima Khamis wameishauri Wizara ya mawasiliano kuwazingatia watu wenye ulemavu wakati wa ujenzi wa barabara ili kuwa na mazingira rafiki ya kuweza kufika skuli.
Kongamano la siku moja lililowashirikisha wadau wa kutetea haki za watu wenye ulemavu ambapo kauli m biu ni “hakuna linalotuhusu sisi pasi na sisi”.