Kiwandani wajifungulia nyumbani, ukosefu huduma ya maji kituo cha afya watajwa
22 September 2023, 2:26 pm
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya katika kuboresha huduma ya mama na mtoto miongoni mwao ni kuweka vituo vya afya lakini bado ni ndoto kwa wakaazi wa Wesha Kiwandani kwani kituo hicho hakina huduma ya maji jambo linalopelekea kujifungulia nyumbani.
Na Khadija Yussuf
Kukosekana kwa maji safi na salama katika kituo ch afya Wesha Chake Chake Pemba ni sababu inayopelekea mama wajawazito kujifungulia majumbani badala ya kukimbilia kituo cha afya.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kiwandani Wesha wamesema wamekuwa wakipata usumbufu wakati wanapokwenda kujifungufua, kwani wanalazimika kubeba ndoo za maji kutoka majumbani kwao jambo linalohatarisha usalama wa mama na mtoto na kuona ni bora kujifungulia majumbani.
Wananchi Asha Omar ambaye ni mama mjamzito na Subira Iddi Ali wamesema wanategea maji kutoka Mamlaka ya Maji Zawa, lakini ni zaidi ya miezi mitatu huduma hiyo haipatikani, hali inayosababisha kushindwa kujifungulia kituoni hapo na badala yake kujifungulia majumbani na wengine kukimbilia Hospitali ya wilaya Chake Chake.
Akizungumgumzia kuhusiana na changamoto hiyo Said Mohd Ali amesema wanalazimika kubeba madumu ya maji wanapowasindikiza wenza wao kituo cha afya wakati wa kujifungua kituoni hapo.
Muuguzi Mkuu wa kituo hicho Amina Ali Abdi amesema kisheria muuguzi anapomaliza kuzalisha anatakiwa anawe kwa maji tiririka ili ajikinge na magojnwa ya mambukizi kutoka kwa mama anaemzalisha.
Daktari dhamana kituo cha afya Wesha Abdulnassir Hemed Said amesema kutokana na ukosefu wa maji kwa mwezi wanazalisha wajawazito 9 tu, kwani wengi wao hujifungulia majumbani.
Afisa uhusiano wa Mamlaka ya Maji Zawa Pemba Suleiman Anass Massoud amekiri kuwepo kwa tatizo la maji kituoni hapo na kusema chanzo kikubwa kinachopelekea kukosa maji baadhi ya wananchi hujiungia maji kiholela kinyume na utaratibu uliowekwa.
Mratibu wa mradi wa kuendeleza utetezi wa vyombo vya habari juu ya haki ya Afya ya Uzazi kwa wanawake na wasichana Zanzibar Zaina Abdala Mzee amesema lengo la kufanya ziara ya kutembelea vituo vya afya ya mama na mtoto, ni kutathmini hali ya utolewaji wa huduma na kusikiliza changamoto ili kuongeza ushawishi na utetezi kupitia vyombo vya habari na kuona huduma za afya ya uzazi zinapatikana.
Ziara hiyo iliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar Tamwa kwa kushirikiana na maafisa kutoka Tume ya Ukimwi, Kitengo shirikishi cha Afya ya mama na mtoto na Wandishi wa habari, ambapo wametembelea kituo cha Afya Wesha, Mgelema,Pujini na Vikunguni katika wilaya ya Chake Chake Pemba.