Ukosefu wa maji kuwanyima wanawake usingizi kijiji cha Mjini Kiuyu
22 August 2023, 12:15 pm
Upatikanaji wa maji bado ni changamoto kubwa katika maeneo mengi Pemba hasa vijijini, jambo ambaolo linawakosesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kikamilifu.
Na Fatma Hamad.
Ukosefu wa huduma za maji safi na salama bado ni kilio kikubwa kwa wananchi wa kijiji cha Mjini Kiuyu wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazi Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwao, Bikame Bakar Darusi, amesema huu ni mwaka wa tano sasa wamekuwa wakikosa huduma hiyo ya maji safi na salama na kushindwa kupata maji ya kutosha ya kufanyia shughuli zao za nyumbani.
Bakar Hamad ikiwa ni moja ya mwanakijiji amesema suala la maji limekuwa ni tatizo sugu ambalo linawatesa wanawake wa kijijini hapo na pia hutoka kwa baadhi ya mabomba wakati wa majira ya saa tano hadi tisa za usiku, hali ambayo inapelekea wanawake kukesha kwenye foleni ya maji.
Fatma Ali na Asha Juma wanafunzi wa darasa la tano wamesema hali hiyo inawapelekea kukosa vipindi vya mwanzo vya masomo darasani kutokana na kuchelewa kwenye kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Afisa uhusiano wa Mamlaka ya Maji [Zawa] Pemba Suleiman Anas Masoud, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kijijini hapo.
Amesema tatizo hilo linasababishwa na kukosekana kwa matangi ya kuhifadhia maji pamoja na uchakavu wa miundombinu ya kusambazia maji.
Masoud amewataka wananchi hao kuwa na subra, kwani tayari wameshaingizwa kwenye mradi mpya ambao unamaliziwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, unaofadhiliwa na benk ya watu wa Ujerumani, ambao utajenga matangi kwenye vijiji vilivyo na shida ya maji.