ZAFELA kuwarudhisha watoto wa kike shule
21 August 2023, 3:20 pm
Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar yapania kuwarejesha skuli watoto wa kike waliokatisha skuli wakiwa bado hawajafikia umri wa kumaliza kwa kushirikiana na taasisi za serikali na NGOs.
Na Fatma Hamad
Asasi za kiraia zimetakiwa kushirikiana kwa pamoja katika kuwajengea uwezo Watoto wa kike, walioacha Skuli ili kuendelea na masomo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA Jamila Mahmud wakati akiutambulisha mradi wa Malala, utakaoendeshwa na Zafela visiwani Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja.
Amesema kwa mujibu wa utafiti walioufanya waligundua kuna wimbi la watoto wa kike waliokatisha masomo yao kutokana na kuolewa, mimba za utotoni pamoja na kufanyishwa kazi za nyumbani.
Mapema msimamizi wa mradi Hairun Abass Rajab kutoka chama cha wanasheria wanawake Zanzibar [Zafela] ameeleza kuwa hadi sasa bado zipo familia ambazo hazimpi fursa mtoto wa kike kupata haki yake ya elimu kuanzia Msingi hadi Vyuo vikuu.
Mwanaharakati wa kulinda na kutetea haki za wanawake na Watoto kutoka Wilaya ya Mkoani Sada Moh’d Othman amesema ni vyema kuweko na mkakati Madhubuti ya usimamizi wanafunzi hao na tusichukulie kuwa umaskini ni sababu ya kutowasomesha watoto wakike.
Mradi huo wa mwaka mmoja umelenga kuwafikia jumla ya watoto 3,000 kwa Unguja na Pemba wenye lengo wa kuwarudisha watoto wakike skuli.