Katibu Machigini: wakulima ongezeni bidii kuondoa uhaba wa chakula
21 September 2022, 11:47 am
Wakulima wa kilimo cha umwagiliaji wa bonde la machigini, shehia ya mjimbini Mkoani Pemba wameshauriwa kuongeza bidii kwenye kilimo chao cha mpunga kwa lengo la kuongeza kasi ya uzalishaji .
Ushauri huo umetolewa na katibu wa bonde hilo,Hamdu Hassan Bakari wakati wa mkutano na wakulima hao, wenye lengo la kujadili jinsi gani wataweza kuongeza uzalishaji katika ukulima wao ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa chakula ambapo taaluma ya kilimo cha kisasa walionayo inaweza kusaidia kufikia malengo hayo.
Amesema wakati umefika kwa wakulima kuacha kulima kwa mazoea na badala yake wafuate maelekezo ya wataalam (mabwana shamba)ili kuongeza kasi ya uzalishaji na kujikwamua na hali duni za kiuchumi pamoja na kuongeza pato la taifa kwa jumla.
Hasina Ali Mussa na Issa Nassor Issa miongoni mwa wakulima wa bonde hilo wamesema licha ya juhudi wanazichukuwa kwenye kilimo chao cha mpunga lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa maji inayosababishwa na miundo mbinu, kutokua sawa kwa baadhi ya maeneo ya bonde hilo hali inayo waweka katika wakati mgumu kwani kilimo chao ni cha umwagiliaji zaidi.
Wakulima hao hivi karibuni walipatiwa msaada wa waya wa umeme na watu wanaoishi nje ya nchi wanaotoka Wilaya ya Mkaoni kwa ajili kurudisha huduma ya maji ili wapate kuendelea shughuli zao za umwagiiaji baada ya kuibiwa waya wao wa mwanzo katika bonde hilo.
Aidha wameiomba Wizara ya kilimo kupitia idara ya umwagiliaji kufika katika bonde lao mara kwa mara ili kuwatatulia changamoto zinazowakabili kama vile kuwapatia wataalamu wakilimo pamoja na vifaa vya kisasa ili kuongeza uzalishaji.
Bonde la machigini lina jumala ya wakulima 200 ambao wanajishughulisha na kilimo cha mpunga wa umwagiliaji na mazao mengine ya biashara kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.