CUCoM sasa ni chuo kikuu
2 January 2024, 17:20
Mwandishi wa Habari
Highlands fm Radio
Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU) imekipa hadhi ya kuwa chuo Kikuu, Chuo cha kanisa Katoliki (Cucom), Kwa sasa kitatambuliwa kama Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUCoM).
Awali chuo hicho kilikuwa kishiriki na chuo cha Mtakatifu Agustino Mwanza kabla ya kuwa na hadhi ya kutambuliwa kama Chuo kinachojitegemea ‘Cucom’.
Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, askofu wa Jimbo Katoliki la Mbinga John Ndimbo imefafanua kuwa TCU, imekipa hadhi ya kuwa chuo Kikuu kuanzia mwaka huu 2024.
Imeeleza kuwa Kwa sasa chuo kicho hicho kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC) kinatambuliwa Kwa Jina la ‘CUCoM’ kuanzia Januari Mosi,2024.
Akizungumza na Highlands Fm, Mkutubi msaidizi wa chuo hicho, Isaya Myoka amesema chuo hicho kimepandishwa hadhi kwa kuwa kina miundombinu Bora, akidi ya wafanyakazi wenye sifa na uwezo wa kijiendesha.
Amesema uwepo wa chuo hicho ni fursa ya Watanzania kupata elimu ya juu, kwani kimejipambanua kupitia program mbalimbali zilizopo, na kwamba Kwa sasa kuna kina sifa hata ya kufungua matawi kulingana na uhitaji.