Highlands FM
Highlands FM
19 June 2025, 10:25

Kumekuwa na changamoto ya wanyamapori wakali ambao wamekuwa wakisababisha madhara kwa jamii TAWA inatoa mbinu kukabiliana nao
Na Samwel Mpogole
Katika jitihada za kulinda maisha ya watu na mali zao, wananchi wametakiwa kuwa makini na kuchukua hatua za haraka kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapowaona wanyama pori wakali kama tembo, simba au viboko wakizagaa katika makazi yao.
Hayo yamesemwa na Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Lembolos Ole, amesema moja ya majukumu ya TAWA ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuishi kwa uhusiano mzuri na wanyama pori, sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Akizungumzia namna ya kukabiliana na wanyama wakali kama tembo, simba na viboko, Afisa huyo ameshauri wananchi kupanda mazao ambayo si kivutio kwa wanyama hao, kuweka uzio utaofanya wanyama isiwe rahisi kuvuka , na zaidi kutoa taarifa haraka wanapowaona wakiingia kwenye makazi ya watu.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya wamesema wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa kutokana na wanyama pori kuvamia mashamba yao, hali inayosababisha uharibifu wa mazao na athari za kiuchumi na kisaikolojia.
Serikali kupitia taasisi zake, inaendelea kuhimiza wananchi kujielimisha kuhusu mbinu sahihi za kuzuia na kukabiliana na wanyama pori, huku ikisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya jamii na mamlaka husika kwa ajili ya kulinda maisha na mali za wananchi.