Highlands FM

Mwanafaunzi wa MUST ashikiliwa kwa tuhuma za mauaji

17 June 2025, 16:31

SACP Benjamini Kuzaga. Picha na Mwandishi wetu

Uhasama wa usiku mmoja umegeuka kuwa msiba wa maisha kwa familia ya mwanafunzi aliyeuawa kwa kuchomwa na mwenzake katika kumbi ya burudani Mbeya

Na Samwel Mpogole

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Emilian Joseph Duzu (21), kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzake wa mwaka wa tatu, Gerald Philbert Said (22).

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamini Kuzaga amesema Tukio hilo limetokea Juni 14, 2025 majira ya saa 11 alfajiri katika Klabu iitwayo Mbeya Pazuri iliyopo Jijini Mbeya, ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimchoma marehemu kwa kitu chenye ncha kali tumboni, hali iliyosababisha majeraha makubwa.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linamshikilia Seven Kipara (38), mkazi wa Ipwizi, kwa tuhuma za kupanga njama za kumuua mama yake mzazi, pamoja na kumjeruhi kwa risasi mtoto wa miaka minne aitwaye Sinzo Jifwalo, mkazi wa kijiji cha Ipwizi.

Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa litachukua hatua kali dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa sheria na linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pale panapohisiwa dalili za uhalifu.

MWISHO.