Highlands FM
Highlands FM
10 June 2025, 11:02

TACOGA 1984 yaweka mkazo kwa ushauri rafiki na wa kisasa kwa wanafunzi wa vyuo
Na Samwel Mpogole
Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984) kimetoa mafunzo kwa washauri wa wanafunzi kutoka vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya kati, vyuo vya ufundi pamoja na viongozi wa serikali za wanafunzi, kwa lengo la kuwaongezea uelewa na uwezo wa kuwapa ushauri wanafunzi na kuwasimamia kwa tija.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Eden jijini Mbeya, yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo afya ya akili, afya ya uzazi pamoja na mbinu bora za ushauri kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Akifunga mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya (CUoM), Profesa Romuald Haule, amewasisitiza washiriki kutumia mbinu rafiki katika kutoa ushauri badala ya kutumia njia ngumu zinazoweza kuwatenga au kuwavunja moyo wanafunzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TACOGA 1984, Bi. Sophia Nchimbi, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za chama hicho kuhakikisha kuwa washauri wa wanafunzi wanakuwa na ujuzi wa kisasa unaoendana na changamoto za sasa zinazowakumba wanafunzi.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayowamesema yamekuwa chachu ya mabadiliko kwao, si tu kwa kuwaongezea maarifa ya ushauri na uongozi, bali pia kwa kuwapa nafasi ya kutafakari nafasi yao katika kusaidia wenzao ndani ya taasisi za elimu ya juu.
Mafunzo hayo yanatajwa kuwa sehemu ya mikakati ya TACOGA 1984 katika kuboresha huduma za ushauri na uongozi kwa wanafunzi katika taasisi za elimu nchini.