Highlands FM
Highlands FM
4 June 2025, 18:57

Waandishi wa habari wamehimizwa kushiriki katika mapambano dhidi ya Rushwa hasa Taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu
Na Samwel Mpogole
Taaisisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa mbeya imewataka waandishi wa habari kushirikiana nao bega kwa bega, hasa katika kipindi hiki Taifa linapoelekea katika Uchaguzi Mkuu.
Hayo yamesemwa na Maghela Ndimbo, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya, alipokuwa akizungumza na Highlands Fm. Ndimbo amesema ushiriki wa waandishi wa habari ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, kwani vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuelimisha umma na kufichua maovu.
Kwa upande wake, Felix Mwakyembe, mwanahabari mkongwe, ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwa makini dhidi ya matumizi ya akili mnemba, kwani kutoitumia kwa umakini inaweza kuharibu mchakato wa uchaguzi na hata kuwaingiza matatizoni.
Katika hatua nyingine, Ndimbo amewataka wananchi kwa ujumla kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa mapema pindi wanapohisi au kushuhudia viashiria vya rushwa.
TAKUKURU inaendelea na juhudi zake za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kwa njia ya haki na uwazi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unakuwa huru na wa haki