Highlands FM
Highlands FM
27 May 2025, 20:11

Kufuatia kuibuka kwa matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (Artificial Intelligence – AI), waandishi wa habari wametakiwa kuwa waangalifu katika kutumia teknolojia hiyo, ili kuepuka kusambaza taarifa zisizo sahihi
Na Samwel Mpogole
Waandishi wa Habari wa Radio za kijamii wametakiwa kuwa waangalifu na matumizi ya akili mnemba ili kuepuka kusambaza habari zisizo sahihina kuleta taharuki kwenye jamii.
Awali, akizungumza katika mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika mkoani Mbeya na kuwahusisha wahariri kutoka vituo mbalimbali vya habari nchini, Afisa Utawala wa TADIO, Fatuma Mahendeka, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa uangalifu na kwa manufaa ya jamii ili kuleta tija na mabadiliko chanya katika taifa.
Hilary Batungwa, ambaye ni mkufunzi na Mhariri wa Radio Tadio amesema kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuuu wa hapa nchini waandishi wa habari wanapaswa kuongeza umakini ili kuepuka migongano isiyo na ulazima na kusisitiza umakini katika akili mnemba.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kwamba mafunzo waliyoyapata yatawasaidia katika kuhabarisha jamii na kuelimisha wananchi kwa ustadi wa hali ya juu.
Ikumbukwe kuwa Radio Tadio ni jukwaa la usambazaji wa habari kutoka redio za kijamii zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar lililoanzishwa rasmi mwaka 2020 likijumuisha zaidi ya vituo vya redio 47 vinavyochapisha habari kila siku.