Highlands FM
Highlands FM
22 May 2025, 23:04

Jeshi la Polisi mkoani Songwe lime kamata silaha mbili aina ya bastola katika oparesheni inayoendelea ya misako na doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hatua inayolenga kukabiliana na matukio ya uhalifu.
Na samweli mpogole
Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, SACP Augustino Senga, amesema bastola ya kwanza imekutwa imetelekezwa katika eneo la maegesho ya magari la Majengo, Mji wa Tunduma, ikiwa ndani ya boksi lake, pamoja na makasha matatu ya risasi zenye jumla ya risasi 150.

Bastola hiyo mpya ni aina ya Retay G91C yenye namba R1YGCMOYO1-2400425 Cal.9mm, rangi nyeusi, na imebainika kuwa imeingizwa nchini kinyume cha sheria.

Katika tukio jingine, Kamanda Senga amesema silaha ya pili iliyokamatwa ni aina ya CZ92 Browning yenye namba A.428007, Caliber 6.35mm, ikiwa na risasi sita zenye rangi ya dhahabu na nyeusi. Silaha hiyo iliibwa kufuatia tukio la uvunjaji wa nyumba lililotokea eneo la Haloli, Wilaya ya Mbozi, ambapo nyumba ya Bwana Emmanuel Fungo ambaye ni mmiliki halali wa silaha hiyo ilivunjwa.
Silaha hiyo ilikamatwa katika eneo la soko la Black Tunduma, ingawa mtuhumiwa alifanikiwa kukimbia, na sasa msako mkali unaendelea ili kuhakikisha anapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kamanda Senga amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na uhalifu, na ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha vitendo vya kihalifu katika mkoa huo.
