CST yatenga Sh 2b kupiga jeki elimu Nyanda za Juu Kusini
21 March 2024, 14:57
Na Lameck Charles
Highlands Fm Radio Mbeya
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Chilid Support Tanzania imezindua mradi wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 mradi wa “Peleka Rafiki zangu Shule” mradi unaolenga kuendelea kutoa mafunzo ya elimu kwa walimu na jamii kwa ujumla.
Akizungumza na wadau wa elimu kutoka mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi Mkurugenzi wa Child Support Tanzania (CST) Bi Noela Msuya amesema mradi huu utahudumu kwa muda wa miaka minne huku akitaja hatua kadhaa zilizotekelezwa na mradi huo tangu kuanza kwake mwishoni mwaka mwaka jana.
Mradi huo uliofadhiliwa na watu wa Ujerumani kwa kushirikiana na CBM unatekelezwa na Child Support Tanzania umefanikiwa kuwafikia watoto zaidi ya elfu moja huku zaidi ya shule 50 zikinufaika na mafunzo ya elimu jumuishi.
Mafunzo ya eilmu jumuishi yatawasaidia wazazi,walezi na jamii katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu haki ya elimu hususani kwa watoto wenye ulemavu..
Pamoja na hayo Bi Noela Msuya ametaja changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya elimu jumuishi ikiwemo miundombinu isiyo rafiki kwenye shule mbalimbali, upungufu wa wataalam wa elimu jumuishi na changamoto ya mitihani kwa watoto wenye ulemavu huku akiiomba serikali kuangalia chanagamoto hizo kwa jicho la pili.
Ni zaidi ya miaka 15 sasa tangu kuanzishwa kwa shirika la Child Support Tanzania lenye makao makuu yake Iwambi jijini Mbeya likiwahudumia watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo kupata haki ya elimu.