Shule mpya wilayani Chunya kuwakomboa wanafunzi
4 January 2024, 14:07
Tayari tumekwisha Jenga vyumba 8 vya madarasa, ofisi za walimu mbili, jengo la utawala, maktaba, jengo la kompyuta na maabara tatu ya kemia, fizikia na biolojia
Na Samwel Mpogole
Shule mpya ya Sekondari ya Kata Kambikatoto wilaya ya Chunya Jimbo la Lupa Mkoa wa Mbeya inayotarajiwa rasmi kuanza masomo muhula wa kwanza January inakwenda kuwakomboa wanafunzi kwa kufuata elimu umbali mrefu wa km 98 kutoka Kambikatoto Mpaka Isangawana, Hali iliyokuwa inachangia wanafunzi kuacha masomo, utoro na mimba za utotoni na baadhi ya Wazazi kushindwa kumudu gharama.
Afisa mtendaji Kata Nicholous Ndongosya ametoa taarifa kwa Mbunge wa Jimbo Masache Kasaka kuwa tayari wamekwisha Jenga vyumba 8 vya madarasa, ofisi za walimu mbili, jengo la utawala, maktaba, jengo la kompyuta na maabara tatu ya kemia, fizikia na biolojia.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo la Lupa Masache Kasaka ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kutoa fedha za miradi inayokwenda kutatua changamoto za wananchi.
Wazazi ambao ndio walikuwa sehemu ya waathirika kwa kukosekana kwa shule katika eneo lao wamesema baadhi yao iliwalazimu kuwasihi watoto wao wafanye vibaya katika mitihani Ili kukwepa gharama za kuwapeleka mbali na makazi Yao kupata elimu.