Uyole watumia vichaa kutupa taka mitaroni
4 December 2023, 17:46
Na Samwel Ndoni
Baadhi ya wakazi wa bonde la Uyole jijini Mbeya wanadaiwa kuwatumia watu wenye ulemavu wa akili ‘vichaa’ kutupa taka kwenye makazi ya watu na mitaro huku wakiwalipa ujira wa sh.500.
Hatua hiyo inatajwa kukwamisha juhudi za usafi wa mazingira kwenye bonde hilo.
Hayo yameelezwa na Diwani wa kata ya Uyole Daniel Njango wakati wa zoezi la kampeni ya usafi wa mazingira lililoandaliwa na Kituo cha Radio ya Kijamii, Highlands Fm, wakishirikiana na halmashauri ya jiji la Mbeya.
Njango amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mbinu ya kuwatumia ‘vichaa’ kutupa taka ili kuepuka kukamatwa na mamlaka za serikali za mitaa hatua aliyoitaja kuwa ni kikwazo cha usafi wa mazingira kwenye eneo hilo.
“Lakini huwa tunawakamata na kuwataka watupeleke sehemu waliyotumwa, baada ya kuwabaini wanaowabebesha mizigo huwa tunawatoza faini kulingana na Sheria zetu za halmashauri” alisema
Katika hatua nyingine alisema Kampeni hiyo ya usafi itakuwa chachu ya kuhamasisha zoezi hilo kufanyika mara Kwa mara huku akieleza kuwa imekuja Kwa wakati Kwa kuwa kipindi hiki ni msimu wa mvua.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya usafi wa mazingira ambayo imepewa Jina la Mvua sio Janga, safisha mazingira, Lameck Charles amesema zoezi hilo litakuwa ni endelevu.