RC Mbeya: Msiwasahau watoto wa kiume, wanapitia ukatili wa kutisha
24 November 2023, 14:59
Na Samweli Ndoni
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amewakumbusha wadau wa sheria na vyombo vya utoaji haki nchini kuelekeza nguvu zao kwenye mapambano dhidi ya ukatili anaopitia mtoto wa kiume akieleza kuwa kampeni nyingi zimewaacha nyuma na badala yake zimejikita kumkomboa mtoto wa kike peke yake.
Amesema hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa suala la ukatili kuwageukia watoto wa kiume, kutokana na wadau wengi wa sheria na vyombo vya utoaji haki kutowekeza nguvu za kutosha kwenye kundi hilo
Akizungumza jijini Mbeya wakati akifunguo mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wa kupambana na ukatili wa wanawake na watoto kwa majaji na mahakimu wanawake wa mikoa ya Mbeya na Songwe, katibu tawala wa mkoa wa Mbeya Lodrick Mpogole amesema nguvu ya pamoja inahitajika ili kuwalinda watoto
Mpogole ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa mbeya, Juma Homera kwenye uzinduzi wa mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na chama cha Majaji na mahakimu wanawake (TAWJA), aliwapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhakikisha matukio ya ukatili wa watoto na wanawake yanapungua
“Nisema tu hapo nyuma tulipokuwa tunazungumzia habari ya ukatili, tulikuwa tukigusa wanawake na watoto, nimefarijika kupitia hotuba hii ya mheshimiwa mkuu wa mkoa, tumemzungumzia mtoto kwa ujumla wake, yaani wa kike na wakiume, inawezekana tumewekeza nguvu sana kwa mtoto wa kike kuliko wa kiume’’ alisema Mpogole
Kwa upande wake, Makamu mwenyekiti wa TAWJA, jaji wa mahakama kuu kanda ya Mbeya, Victoria Nongwa amesema Tanzania imefanya vizuri kwenye medani za kimataifa katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu haki za watoto na wanawake