Wanahabari Mbeya wapewa mbinu za kukabiliana na majanga ya moto
17 November 2023, 16:56
Na Mwanaisha Makumbuli
Wanachama wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mbeya, (MBPC) wamepewa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto ili kuwajengea uwezo wa kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya majanga hayo.
Pia mafunzo hayo ya siku moja yaliyotolewa na jeshi la zimamoto na uokoaji yatawawezesha waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya kuripoti taarifa za majanga bila kuleta taharuki kwenye jamii na kuondoa mtazamo hasi kuwa jeshi la zimamoto na ukoaji halitimizi wajibu wake ipasavyo.
Akitoa mafunzo hayo, Afisa habari wa jeshi la zimamoto na uokoaji, koplo Esther Kinyaga amesema wameamua kutoa elimu kwa waandishi wa habari kwa kuwa kundi hilo lina nafasi ya kufikia jamii kwa urahisi.
Aidha, amesema suala la kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwenye taasisi na vikundi ni sehemu ya mpango jeshi hilo na kwamba hatua hiyo imelenga kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya moto kwenye jamii.
Nao baadhi ya waandishi wa habari wamesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yamewajengea uwezo wa namna ya kufikisha taarifa kwa wananchi juu ya kujikinga na majanga ya moto
Jeshi la zimamoto na uokoaji nchini Tanzania limekuwa likitoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimba nchini namna ya kujikinga na majanga ya moto pale tu tatizo linapotokea.