Wanafunzi marufuku mikesha ya ngoma(sherehe) za usiku
27 September 2023, 13:07
Baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwahusisha watoto wadogo kwenye sherehe hali inayopelekea watoto kubadilika tabia na wengine kushindwa kuendelea na masomo na kuwa wanenguaji katika sherehe hizo.
Na Samwel Mpogole
Afisa Tarafa wa Sisimba Jijini Mbeya John Mboya amewataka wazazi na walezi kata ya Itagano Jijini Mbeya kuzingatia suala la elimu na kutowaruhusu wanafunzi kushiriki kwenye sherehe za usiku lakini pia kukemea utoro katika baadhi ya shule zinazopatikana ndani ya kata hiyo.
Hayo ameyaeleza akiwa katika ziara zake za kupitia na kukagua hali ya taaluma katika kata hiyo na kugundua kuwepo kwa utoro na wazazi kutosimamia suala la elimu kwa watoto wao hali inayoweza kupelekea kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Pia ametoa rai kwa wanafunzi hao kuhakikisha wanafuatilia masomo yao vizuri ili waweze kutimiza ndoto zao lakini pia amewataka wazazi kuhakikisha wanawafatilia watoto wao katika masomo yao.
Ziara hiyo inalenga kutatua changamoto zilizopo katika suala la elimu kata ya Itagano iliyopo Tarafa ya Sisimba na kuzungumza na watumishi waliopo katika kata hiyo.