Wanawake Hai watakiwa kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
5 March 2024, 1:33 pm
Wanawake wilayani Hai wametakiwa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inayotarajiwa kuadhimishwa Machi 8 mwaka huu.
Na Elizabeth Mafie
Wanawake wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujitokeza kushiriki katika kusherehekea siku ya wanawake duniani yanayotarajiwa kufanyika kiwilaya Machi 8, 2024 kata ya Machame Narumu .
Kadhalika wanawawake wametakiwa kushiriki na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali za mitaaa, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) wilaya ya Hai Happiness Eliufoo wakati akizungumza na wanawake wa wilaya ya Hai katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi CCM.
Kwa mujibu wa Eliufoo, wanawake wanatakiwa kuwekeza kwenye usawa wa kijinsia ambapo amesema wanawake wanatakiwa na kushiriki katika chaguzi mbalimbali za kiserikali.
Amesema wanawake wanapokwenda kuadhimisha siku hiyo wanatakiwa kuhamasishwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kupata viongozi wanawake wa kutosha.
Aidha amesema katika takwimu za uongozi wanawake ni wachache tofauti na wanaume ambapo amewashauri wanawake kuwekeza katika elimu, uongozi na kuwasaidia waliopo chini na kuacha tabia ya kukatishana tamaa katika mambo mbalimbali ili waweze kufikia ngazi ya maamuzi na kuwekeza katika usawa .
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Upendo Sawe amewataka wanawake kuwa mabalozi wa kuhamasishana kujitokeza kwa wingi katika kusherehekea siku ya mwanamke duniani.
Naye katibu wa siasa uenezi na mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Hai Mohamed Msalu amesesisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika siku hiyo ya wanawake.
Siku ya mwanamke duniani huadhimishwa kila mwaka mwezi Machi na wanawake kutoka Tanzania hukutana na kuadhimisha siku hiyo na kujengeana uwezo katika mambo mbalimbali .