Savvy FM

Teknolojia ipewe kipaumbele kwenye ukusanyaji kodi: Mhe Ndejembi

6 October 2026, 9:18 pm

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akifungua Mkutano wa 46 wa chama cha wasimamizi wa mamlaka za kodi wa jumuiya ya madola (CATA)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesisitiza matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia katika ukusanyaji wa kodi nakusema yanapaswa kutiliwa mkazo ili kuongeza uwazi, kuimarisha usimamizi wa kodi na kurahisisha ulipaji kodi na kutaka mijadala ya mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) uangazie zaidi teknolojia.

Na Mariam Mallya

Akifungua Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Mamlaka za Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), unaofanyika katika Ukumbi wa Grand Melia Arusha leo Jumanne Oktoba 06, 2026 Mhe. Ndejembi amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuimarisha huduma kwa walipa kodi ndiyo maana mkutano huo umekuja na kauli mbiu inayogusa teknolojia.

Amesema pamoja na umuhimu wa teknolojia, mafanikio katika ukusanyaji wa mapato hayawezi kutegemea teknolojia pekee, bali yanahitaji sera nzuri, madhubuti, zinazoeleweka na zinazotabirika, pamoja na usimamizi wa kodi wenye ufanisi na unaokidhi mahitaji ya walipakodi.

Makamu wa Rais pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, akibainisha kuwa biashara zinazovuka mipaka, makampuni ya kimataifa, miamala ya kidijitali pamoja na mali za kifedha zinazohifadhiwa nje ya nchi zimefanya ushirikiano kati ya mamlaka za kodi kuwa muhimu zaidi.

Amesema Tanzania inaendelea kuimarisha ushiriki wake katika ushirikiano wa kimataifa wa kodi, ikiwemo kubadilishana taarifa za kodi na kutoa msaada wa kiutawala baina ya nchi huku akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza uhakika wa kodi, kubadilishana taarifa, kuzuia na kutatua migogoro ya kikodi.

Aidha Makamu wa Rais amesema mifumo ya kodi inatakiwa kusaidia na si kuzuia shughuli za uzalishaji kiuchumi, kwa kutoa uhakika, kurahisisha biashara halali, kuhamasisha uwekezaji na kurasimisha shughuli za kiuchumi nchini , huku akibainisha kuwa mfumo mzuri wa kodi unapaswa pia kuiwezesha sekta binafsi kutekeleza nafasi yake muhimu katika uwekezaji, uzalishaji, uanzishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza katika mkutano wa CATA.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ambayo yameboresha zaidi huduma za usimamizi wa kodi kwa kuongeza uwazi na ufanisi.

Amesema kupitia matumizi ya teknolojia TRA imekuja na mfumo wa IDRAS unaosimamia kodi za ndani ambao unamuwezesha Mlipakodi kutoa risiti za kielektroniki kwa kutumia simu ya mkononi bila kuwa na mashine hali ambayo imeongeza uhiari katika kulipa kodi na kupunguza kuonana kwa walipakodi na maofisa wa TRA.

Amesema kupitia mkutano huo wataweza kubadilishana ujuzi na mataifa mengine akieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa pia kwa Tanzania yameongeza wigo wa kodi kutokana na kuwapa uhuru walipakodi kujisajili kupitia mtandao na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN).

Mkutano huo unalenga kuangalia namna teknolojia inavyoweza kutumika si tu kuongeza mapato ya serikali, bali pia kuboresha utoaji wa huduma na kujenga mifumo ya kodi iliyo bora, yenye uwazi na inayoweza kukidhi mahitaji ya wakati huu.