Savvy FM
Savvy FM
8 October 2026, 12:59 pm

Wananchi wanaoishi katika maeneo ya Morombo na Intel jijini Arusha wamelalamikia changamoto ya usafiri inayotokana na ujenzi wa barabara unaoendelea katika maeneo hayo.
Wakazi hao wakiwemo wafanyabiashara wanaokaa katika maeneo hayo wamesema hali hiyo imekuwa kikwazo katika shughuli zao za kila siku huku baadhi ya abiria wakilazimika kutumia maguta kama njia mbadala ya usafiri ili kufika katika makazi yao.
Changamoto hiyo imeonekana kuwa kubwa zaidi kwa wanafunzi, ambapo baadhi yao wamedai kukumbana na ugumu wa kupata usafiri kutokana na baadhi ya makondakta wa daladala kuwapa kipaumbele abiria wanaolipa nauli kubwa, badala ya wanafunzi wanaolipa nauli ya shilingi 200.
Akizungumza kuhusiana na changamoto hiyo Mwenyekiti wa umoja wa daladala Mkoani Arusha, Musa Njuga, amesema changamoto hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ujenzi wa barabara ya Kwa Morombo, pamoja na baadhi ya abiria kukosa uvumilivu wa kusubiri daladala wakati magari yakipita kwa shida katika eneo hilo.