Savvy FM

APSP yakazia weledi na uwajibikaji

30 July 2026, 3:07 pm

Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP), Emmanuel Urembo. Picha na Mariam Mallya

Wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini wamehimizwa kuimarisha usimamizi wa vihatarishi katika mchakato wa ununuzi wa umma kwa kubaini mapema sababu zinazoweza kusababisha hasara au ukiukwaji wa sheria.

Na Mariam Mallya

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP), Emmanuel Urembo, wakati wa Mkutano Mkuu wa Tano wa Jukwaa la Kikatiba na Kitaaluma la chama hicho uliofanyika jijini Arusha amesema wataalamu wa sekta hiyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji mkubwa ili kuimarisha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na kuongeza imani kwa wananchi.

Urembo amesema moja ya malengo ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma na Ugavi kwa Sekta ya Umma Afrika ni kuongeza ushiriki wa wazalishaji wa ndani pamoja na biashara ndogo na za kati (SMEs). Mfumo huo pia unalenga kutoa fursa zaidi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki katika zabuni za serikali kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP), Emmanuel Urembo

Kwa upande wake, Katibu wa Mamlaka ya Rufaa za Ununuzi wa Umma (PPAA), James Sando, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za ununuzi ili kuhakikisha uwazi, ushindani wa haki na matumizi bora ya fedha za umma.

Sauti ya katibu wa PPAA James Sando

Akifungua mkutano huo, Mlezi Mkuu wa APSP, Dkt. Frederick Asumile Mwakibinga, amewataka wataalamu wa ununuzi kulinda mipango ya bajeti inayotengwa kwa shughuli za ununuzi wa umma, kuhakikisha ushindani wa haki katika zabuni, kudhibiti migongano ya maslahi pamoja na kutumia kwa ufanisi Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST)

Sauti ya mlezi mkuu wa APSP, Dkt. Frederick Asumile Mwakibinga

Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Kuimarisha Ushiriki wa Kitaaluma, Kuwezesha Makundi Maalumu na Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) Kunufaika na Urasimishaji wa Biashara, Uzingatiaji wa Umiliki Halisi na Fursa za Ununuzi wa Umma Nchini Tanzania.”