Savvy FM
Savvy FM
8 August 2026, 6:46 pm

Wakulima, wazalishaji na wafanyabiashara nchini wametakiwa kujisajili na kupata nembo ya TANTRADE ili kuongeza utambulisho wa bidhaa zao na kuzifanya zitambulike zaidi katika masoko ya kimataifa.
Na Gasper Sambweti
Afisa mwandamizi wa biashara wa TANTRADE, Bw. Thomas Peter Mallya amesema usajili na matumizi ya nembo ya TANTRADE ni hatua muhimu katika kuitangaza Tanzania kupitia bidhaa zenye ubora, kuongeza uaminifu wa wanunuzi, pamoja na kufungua fursa za ushindani katika soko la dunia.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo pia itaongeza thamani ya bidhaa za Tanzania na kuwezesha wazalishaji kupata masoko mapana zaidi ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema TANTRADE inaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa usajili wa bidhaa na nembo ya taifa kwa lengo la kuimarisha biashara, kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania na kukuza uchumi wa nchi.
Kupitia mfumo huo, wafanyabiashara na wazalishaji wanaweza kusajili bidhaa zao na kupata nembo rasmi ya TANTRADE inayotambulisha bidhaa hizo kama bidhaa za Tanzania.
Bw. Mallya ametoa wito huo wakati wa Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya TASO, jijini Arusha, akisisitiza kuwa usajili wa bidhaa ni nyenzo muhimu ya kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.