Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
17 November 2026, 8:51 pm

Vijana wilayani Butiama wamehimizwa kujikita katika ujasiriamali badala ya kusubiri ajira serikalini. Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo ya vitendo ya utengenezaji wa sabuni za maji yaliyoandaliwa kwa wadau na wasikilizaji wa Butiama FM, kwa lengo la kuwajengea ujuzi wa kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Na Amos Marwa
Vijana wilayani Butiama wametakiwa kubadilika kimtazamo na kutumia fursa mbalimbali za ujasiriamali zinazowazunguka ili kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi, badala ya kusubiri ajira serikalini.
Wito huo umetolewa na mwalimu wa wajasiriamali na mwenyekiti wa kundi la ujasiriamali la Fadhira Kwanza wilayani Butiama, Bwana Mzuma Tambwe, alipokutana na wadau wa Butiama FM pamoja na wasikilizaji wa kipindi cha Makala za Biashara na Ujasiriamali. Katika mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kwa vitendo kuhusu namna ya kutengeneza sabuni za maji, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kujiajiri na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wao, wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Butiama FM kwa kuandaa fursa hiyo iliyowawezesha kupata ujuzi mpya wa kivitendo. Aidha, wamewataka vijana wengine kujitokeza kwa wingi na kushiriki mafunzo kama hayo yanapotangazwa ili waweze kupata maarifa yatakayowasaidia kujiajiri na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Mafunzo hayo ya vitendo yamefanyika kufuatia washiriki kupata elimu ya kinadharia kupitia kipindi cha Makala za Biashara na Ujasiriamali kinachorushwa na Butiama FM kila siku ya Jumapili, hatua inayolenga kuwajengea wasikilizaji uelewa na ujuzi wa kutumia fursa za biashara na ujasiriamali katika maisha yao ya kila siku.
