Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
29 August 2026, 9:45 am

“Usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja. Madereva wanapaswa kuzingatia sheria, kuepuka mwendo kasi, ulevi na matumizi ya simu wakati wa kuendesha, pamoja na kuhakikisha vyombo vyao vya usafiri viko katika hali nzuri kabla ya kuanza safari.”Kaimu Mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Butiama Sajenti Merick Mabubi
Na Amos Marwa
Kaimu Mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Butiama Sajenti Merick Mabubi ametaja mwendo kasi, ulevi, uzembe wa madereva na kutofuata sheria za barabarani kuwa miongoni mwa sababu za ajali. Amesema matumizi ya simu wakati wa kuendesha, uchovu wa madereva na kubeba abiria kupita kiasi pia huongeza hatari ya ajali.
Akizungumza kupitia kipindi maalumu cha elimu ya usalama barabarani kinachorushwa kila Jumamosi asubuhi na Butiama FM, amewataka madereva kuzingatia sheria na taratibu za barabarani, pamoja na kukagua vyombo vyao vya usafiri kabla ya kuanza safari.
Kwa upande wa watembea kwa miguu, amesema kutokuwa makini wakati wa kuvuka barabara na kutumia barabara wakiwa wamelewa ni miongoni mwa vihatarishi vya ajali.
Ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuchukua tahadhari na kuzingatia sheria ili kupunguza ajali na kuokoa maisha.
