Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
1 July 2026, 9:15 am

”Timu zilizothibitisha kushiriki mashindano ya Vilevile Cup mwaka huu zimegawanywa katika makundi mawili. Kundi A linaundwa na Bisarye FC, Kigori FC, Muriaza FC na Rwamkoma FC, huku Kundi B likijumuisha Toto Tundu FC, Ikorokomyo FC, Bumangi FC, Vijana Muriaza FC na Bodaboda FC. Mashindano yatafunguliwa rasmi Julai 4, 2026, kwa mchezo wa ufunguzi utakaowakutanisha Bisarye FC dhidi ya Mtuzu FC kwenye Uwanja wa Mwenge uliopo Butiama. Baada ya kuhitimishwa kwa mashindano hayo, bingwa atakabidhiwa kombe na medali, mshindi wa pili atazawadiwa medali, mshindi wa tatu pia atapata medali, huku mchezaji bora wa mashindano, golikipa bora na kocha bora wakitunukiwa tuzo maalum” Kulwa Karedia Jackton mratibu wa mashindano
Na Amos Marwa
Mashindano ya Vilevile Cup, yanayofanyika kila mwaka Wilaya ya Butiama kwa lengo la kuthamini na kutambua mchango wa Jackton Nyambeleka Nyerere, yamezinduliwa rasmi leo, Juni 30, na Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mratibu wa mashindano hayo, Kulwa Karedia Jackton, ambaye ni mwanafamilia wa Jackton Nyambeleka Nyerere, amesema lengo la mashindano hayo ni kukuza vipaji vya vijana, kuzuia vitendo vya uhalifu, pamoja na kuimarisha amani, upendo na mshikamano katika jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Julai 4, wamewashukuru waandaaji kwa kuendelea kuandaa mashindano yanayowapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao, huku yakichochea umoja na ushirikiano katika jamii.
Wakati huo huo, Kamati ya Maandalizi imezitaka timu zote zitakazoshiriki kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa amani, ushindani wa haki na mafanikio.
