Butiama FM Radio

Mbunge aahidi suluhisho la kero Muriaza

19 July 2026, 7:45 am

Mbunge wa Jimbo la Butiama Dkt. Wilson Mahera Charles akizungumza na Wananchi katika moja ya ziara zake za kikazi katika jimbo lake. Picna na Mtandao

‘’Masuala yote yaliyowasilishwa yanaendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na Serikali na mamlaka husika ili kupata suluhisho la kudumu’’ Dkt. Wilson Mahera Charles

Na Amos Marwa

Mbunge wa Jimbo la Butiama Dkt. Wilson Mahera Charles, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Kata ya Muriaza, ambapo amekagua ujenzi wa Shule za Sekondari Mwikoko na Kizaru zinazojengwa kwa ushirikiano wa wananchi na Mfuko wa Jimbo. Pia ametembelea Shule ya Msingi Kizaru na kujionea matumizi ya saruji iliyotolewa na Nyansaho Foundation iliyowezesha uwekaji wa sakafu katika madarasa mawili.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Bumangi, amekutana na walimu na kuwapongeza kwa ufaulu wa wanafunzi, huku akiwashauri kuanzisha mikondo ya PGM, EGM na HGL ili kupanua fursa za masomo na kuwaandaa wanafunzi kwa taaluma mbalimbali.

Katika ziara hiyo, amefanya mikutano ya hadhara katika vijiji vya Kizaru, Bumangi na Muriaza, ambapo amesikiliza kero, changamoto na maoni ya wananchi. Amesema masuala yote yaliyowasilishwa yanaendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na Serikali na mamlaka husika ili kupata suluhisho la kudumu.

Mmoja wa akina Mama katika kata ya Muriaza akiomba majiko ya gesi yenye ruzuku mbele ya Mbunge wa Jimbo la Butiama Dkt. Wilson Mahera Charles ili kuwapa akina mama unafuu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. picha na Mtandao

Dkt. Mahera, amewashukuru wananchi wa Kata ya Muriaza kwa ushirikiano na imani wanayoendelea kumuonesha, na kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Jimbo la Butiama na taifa kwa ujumla.

Mwananchi Kata ya Muriaza kwa niaba ya vijana akitoa pongezi kiwa serikali mbele ya Mbunge wa Jimbo la Butiama Dkt. Wilson Mahera Charles kwa kuwapa vijana mikopo ya asilimia kumi. picha na Mtandao