Butiama FM Radio

Redio za jamii zajengewa uwezo wa kukabiliana na Ebola

8 June 2026, 8:08 am

Mwenyekiti wa mtandao na mwavuli wa kitaifa unaounganisha vituo vya redio za jamii, Tanzania Development Information Organization.(TADIO) John Baptist, akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya redio za kijamii namna bora ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. picha na Rose Haji Mwalimu

Redio za kijamii zinaendelea kuwa daraja muhimu kati ya wataalamu wa afya na wananchi. Kupitia mafunzo haya, tunajenga uwezo wa wanahabari kutoa taarifa sahihi, kuondoa upotoshaji na kuhamasisha jamii kuchukua hatua stahiki za kujikinga,” John Baptist Mwenyekiti wa TADIO

Na Rose Haji Mwalimu

Wafadhili wa miradi mbalimbali nchini wamekumbushwa umuhimu wa kuvishirikisha vyombo vya habari si tu katika hatua za upangaji wa shughuli, bali pia kwa kuvitengea bajeti maalum katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuwezesha uhamasishaji na utoaji wa taarifa sahihi kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Afisa Mawasiliano wa Shirika la Red Cross, Seic Kasuga, wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kuhusu maandalizi na mwitikio dhidi ya ugonjwa wa Ebola yaliyofanyika jijini Dodoma kuanzia Juni 4 hadi 5, 2026.

Kasuga amesema imekuwa kawaida kwa baadhi ya wafadhili na taasisi mbalimbali kuvishirikisha vyombo vya habari katika mipango ya miradi, lakini kushindwa kuvitengea fedha katika bajeti za utekelezaji jambo linalopunguza ufanisi wa shughuli za uhamasishaji kwa jamii.

Mwakilishi kutoka wizara ya afya Grace msemwa akizungumza na watendaji wa redio za kijamii kutoka maeneo mbalimbali nchini walioshiriki mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TADIO . Picha na Rose Haji Mwalimu

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TADIO, John Baptist, amesema redio za kijamii zina nafasi muhimu katika kuifikia jamii kwa haraka, hususan wakati wa majanga ya kiafya kama mlipuko wa Ebola.

Mafunzo hayo pia yamesisitiza umuhimu wa redio za kijamii kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya afya ya umma.

Watendaji wa redio za kijamii kutoka maeneo mbalimbali nchini wameshiriki mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TADIO kwa ushirikiano na UNICEF pamoja na Wizara ya Afya, yakilenga kuimarisha maandalizi na mwitikio dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini

JAMII
Watendaji wa redio za kijamii kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifuatilia kwakaribu mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TADIO. picha na Rose Haji Mwalimu