Butiama FM Radio

Serikali kuboresha Barabara za ndani Butiama

4 July 2026, 7:48 am

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza na wananchi wa wilaya ya Butiama katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mwenge, Butiama. Picha na Yunus Himidi

“Nawataka vijana na wananchi wote kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi, kwa sababu mazingira ya amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Bila amani, hatuwezi kujenga uchumi imara wala kufanikisha maendeleo tunayoyahitaji kama taifa.”Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Na Amos Marwa

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameihakikishia jamii ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara kuwa Serikali itachukua hatua za haraka kuboresha barabara za ndani ambazo zimekuwa hazipitiki, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa pamoja na huduma za kijamii.

Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mwenge, Butiama, Dkt. Nchemba amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha, amemuelekeza Meneja wa TARURA Wilaya ya Butiama kwa kushirikiana na Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara kukamilisha usanifu wa barabara hizo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ili hatua za ujenzi na ukarabati zianze kwa wakati.

Sauti ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akihakikishia jamii ya Wilaya ya Butiama kuhusu maboresho ya barabara ambazo hazipitiki wilaya ya Butiama
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiweka Jiwe la Msingi katika Hospitali ya Wilaya Butiama Kizurira Nyerere. Picha na Yunus Himidi

Waziri Mkuu pia amewataka wananchi wa Butiama kuendelea kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kulinda miundombinu ya umma na kujiepusha na vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuhatarisha usalama na maendeleo ya taifa.

Sauti ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwaataka vijana na wananchi wa Wilaya ya Butiama kuendelea kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi

Ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba mkoani Mara ni ya siku tano, ikiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mwenge Butiama kutoa kero zao kwa Waziri mkuu Mwigulu Lameck Nchemba. Picha na Yunus Himidi